FAIDIKA NA ZOTE KALI KATIKA MSIMU WA SIKUKUU.

FAIDIKA NA ZOTE KALI KATIKA MSIMU WA SIKUKUU.
......................................................................................................................

TUMEKUFIKIA

TUMEKUFIKIA
..............................................

TUUNGANE KWA PAMOJA

TUUNGANE KWA PAMOJA
.............................................................

KIJUKUU BLOG TEAM SISI TUTAWALINDA WEWE JE?

KIJUKUU BLOG TEAM SISI TUTAWALINDA WEWE JE?
...................................................................

KARIBU KAHAMA KWA MALAZI SAFI.

KARIBU KAHAMA KWA MALAZI SAFI.
PLACE TOBE

NJOO UPENDEZE NASI

NJOO UPENDEZE NASI
TUPIGIE 0758-762255

WAUZAJI WA VIFAA VYA SHULE MJINI BUKOBA.

WAUZAJI WA VIFAA VYA SHULE MJINI BUKOBA.
....................................................................

'

'
'

Kwa Habari Makini za Kila siku, Michezo,Burudani,Biashara,Matukio na Habari za Kimataifa tembelea hapa, pia kwa matangazo wasiliana nasi  Piga 0767942570 au 0786942470

Saturday, April 30, 2016

HUU HAPA UKWELI KUHUSU DAWA ZA MSD KUTUMIA MIAKA 4 KUTOKA KEKO KWENDA MUHIMBILI

BOHARI ya Dawa (MSD) imetoa ufafanuzi kuhusu dawa za sh.bilioni mbili kuwa njiani kutoka Bohari ya Dawa ya Keko kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili tangu mwaka 2012.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu alisema hakuna dawa ambazo ziko njiani tangu mwaka 2012 kutoka Bohari ya Dawa kwenda Muhimbili kama ilivyodaiwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Bungeni.

Bwanakunu alisema kuwa ripoti ya CAG ilionesha dawa na vifaa tiba vyenye thamani ya sh.bilioni 2.03 havikuwa vimefika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili tangu Mei 2012 licha ya kuonekana kwenye ankara 23 na Bohari ya Dawa.

"Tunapenda kutoa ufafanuzi kuwa ankara hizo sio kwamba dawa hazikufika hospitalini hapo, bali hazikuonekana kwenye vitabu vya kupokelea mali vya Hospitali ya Muhimbili" alisema Bwanakunu.


Alisema kwamba baada ya kupitia nyaraka zake, Bohari ya Dawa mpaka sasa imefanikiwa kupata uthibitisho wa hati za kupelekea mali za dawa na vifaa tiba vyote vilivyopokelewa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambavyo ni pamoja na dawa za figo na moyo ambazo zilikwishapelekwa Muhimbili.

Aliongeza kuwa pamoja na juhudi za MSD imewasiliana na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ili kuainisha taarifa za kwenye ankara na shehena ya dawa na vifaa tiba vilivyopelekwa hospitalini hapo kwani utaratibu wa kupeleka na kukabidhi dawa hospitalini unamlazimu mpokeaji kusaini ankara ya kupeleka mali ambazo zote zipo MSD.

Akitolea ufafanuzi kuhusu picha zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii za gari aina ya lori lenye herufi "MSD" na kutoa maelezo kuwa ni gari la MSD amesema nembo inayoonekana kwenye gari hilo siyo ya Bohari ya Dawa.

Katika ripoti ya CAG ilionesha kwamba madawa na vifaa tiba ambavyo havikupokelewa kwa muda mrefu kutoka MSD vilikuwa vyenye thamani ya sh.bilioni 2.03 ambapo katika hali ya haikutajiwa kuchukua zaidi ya wiki moja kufikishwa sehemu husika ukizingatia ofisi zao ziko Dar es Salaam.

Rais Magufuli Afungua Rasmi Kikao Kazi Cha Makamanda Wa Polisi....Akerwa na Mikataba Mibovu Inayolidhalilisha Jeshi la Polisi

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amelitaka Jeshi la Polisi nchini na Ofisi ya Mwendesha Mashitaka kujirekebisha kwa kutekeleza wajibu wao huku wakitanguliza maslahi ya taifa.

Rais Magufuli ametoa maagizo hayo jana tarehe 29 Aprili, 2016 wakati akifungua kikao cha kazi cha Makamanda wa polisi wa mikoa, Mawakili wafawidhi wa serikali  wa Mikoa na Wakuu wa upelelezi wa Mikoa na Vikosi, kinachofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa Mikutano wa Dodoma uliopo katika eneo la Tambukareli Mjini Dodoma.
 
Awali kabla ya kutoa hotuba yake Rais Magufuli aliwapa nafasi Makamanda na Mawakili Wafawidhi hao kutoa maoni yao juu ya changamoto zinazowakabili katika kutekeleza wajibu wa kufanya upepelezi na kuendesha mashitaka, hususani kujua sababu za kuchelewesha kesi za makosa ya jinai, ambapo wamedai ufinyu wa bajeti ndio sababu kubwa ya kucheleweshwa kwa kesi za hizo.
 
Kufuatia kutajwa kwa changamoto hiyo Rais Magufuli ameahidi kuhakikisha anawatafutia fedha kwa ajili ya kukabiliana nazo, lakini ametaka fedha zitakazotafutwa zitumike vizuri kwa kuwa taarifa zinaonesha Jeshi la Polisi limekuwa likihusishwa na matumizi mabaya ya fedha hali inayoongeza ukubwa wa matatizo yanayokwamisha utendaji wake wa kazi.
 
Ametolea mfano wa taarifa za matumizi mabaya ya fedha zinazotolewa kwa ajili ya kununulia vifaa na sare za askari, ama mikataba yenye mashaka inayotiwa saini kati ya Polisi na wawekezaji kuwa ni baadhi ya mambo yanayoongeza hali ngumu ya utendaji kazi kwa jeshi hilo.
 
"Oysterbay pale ni eneo ambalo ni very prime, kila mmoja anajua, mmeingia kwenye mikataba mnayoijua nyinyi, akapewa mtu anawajengea pale, sifahamu kama majengo hayo yanafaa. Palikuwa na ubaya gani eneo la Oysterbay likawa na hati, mkaitumia hiyo hati kwenda kukopa benki na kujenga nyumba hata za ghorofa 20 pale, mkaweka investment  na Polisi wenu wakakaa pale. Nimesema lazima nizungumze kwa uwazi, nisiposema kwa uwazi nitajisikia vibaya nikimaliza mkutano huu, nataka muelewe na muelewe ukweli direction  ninayoitaka mimi" Amesema Rais Magufuli
 
Aidha, Rais Magufuli ameitaka Ofisi ya Mwendesha Mashitaka kujipanga kufanya kazi kwa ufanisi na ameelezea kusikitishwa kwake na vitendo vya serikali kushindwa katika kesi nyingi mahakamani licha ya kuwa na wanasheria mahiri.
 
"Niwaombe mawakili na polisi wanaohusika na upelelezi mtangulize maslai ya nchi mbele, kwa sababu kumekuwa na usemi kwa baadhi ya wapelelezi na mawakili wachache, nasema wachache, panapokuwa na kesi inayohusiana na pesa pesa, wana misemo yao wanasema dili limepatikana, na saa nyingine kesi inapopelekwa mahakamani wana-collude Mawakili wa serikali na mawakili wanaomtetea  mhalifu, na wanapo-collude siku zote serikali inashindwa. Unapoona hali hiyo ya kila siku serikali inashindwa, halafu siku hiyo unataka serikali ikuwezeshe, kwa vyovyote serikali inapata kigugumizi" amesisitiza Rais Magufuli.
 
Dkt. Magufuli pia amelitaka Jeshi la Polisi kujiepusha na kashfa ambazo zimekuwa zikisemwa dhidi yake, ikiwemo maafisa wa Polisi kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya na kuazimisha silaha kwa wahalifu wa ujambazi.
 
Hata hivyo Rais Magufuli amelipongeza Jeshi la Polisi na ofisi ya Mkurugenzi wa  Mashitaka kwa kazi kubwa wanayoifanya na ametaka apelekewe mpango wa mahitaji yao ili atafute namna ya kuimarisha vyombo hivyo.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dodoma
29 Aprili, 2016 

UVCCM Wamtaka Fredrick Sumaye Amwache Rais Magufuli Afanye Kazi Yake

Umoja wa vijana wa Chama cha mapinduzi umesema Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye hana vigezo wala sifa zozote zinazoweza kumfanya awe na uwezo wa kumkosoa Rais Dk John Magufuli katika uendeshaji wa serikali na masuala ya utawala.

Sumaye ametakiwa amuache Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dk Magufuli ili atimize majukumu yake kwa sababu alipewa dhamana ya kuwa Waziri mkuu lakini hakufikia hata theluthi ya utendaji unaofanyika sasa.

Msimamo huo umetolewa jana na Kaimu katibu mkuu wa uvccm shaka hamdu shaka alipokuwa akizungumza na wanachama wa ccm wa kata mbili za kwandele na mbichi jimbo la Rombo mkoani kilimanjaro.

Shaka alisema anachokifanya Sumaye na baadhi ya wanasiasa muflis wanaojaribu kukosoa utendaji katika utawala wa serikali ya awamu ya tano ni kutaka nao wasikike wakidhani yale walioyafanya wakati wakiwa madarakani wananchi wameyasahau.

Alisema kama yupo waziri mkuu ambaye ameonyesha udhaifu katika utendaji na usimamizi wa serikaki huku akishindwa kumsaidia Rais hakuna atakayempita Sumaye.

Aidha Kaimu huyo alimuonya Sumaye kuacha kumfuatafuata Dk Magufuli katika mikakati yake ya kutumikia nchi na juhudi anazozichukua dhidi ya mafisadi na wabadhirifu wa mali za umma nchini.

Alisema wakati Rais Magufuli akiwa katika dhamira njema na nia ya wazi kuwatumikia wananchi kwa uadilifu, uaminifu na heshima  kina sumaye na wenzake wafumbe midomo yao na waache mara moja kumbughudhi Rais kwa ajili ya kusaka umaarufu wa kisiasa.

Pia shaka aliwataka wananchi wa jimbo la Rombo kujitayarisha ili kumpiga chini mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya chadema Joseph Selasini kwa sabahu ni dhaifu na hatoshi kuwatumikia wananchi wa jimbo hilo.

"Siku zake za kuitwa mbunge wa Rombo sasa zinahesabika, Selasimi hajui anachokifanya wala hajali shida na matatizo yaliopo katika jimbo lake,lazima adui huyo apigiwe mwaka 2020 "alisisitiza shaka

Akizungumza katika mkutano huo mwenyekiti wa uvccm mkoa wa kilimanjaro Juma Raib Juma aliwakanya wananchi wa kanda ya Kaskazini kuacha mara moja tabia ya kushiriki na kuchagua vyama na wagombea wa nafasi mbali mbali kwa ukabila, ujimbo au nasaba.

Raibu alisema ikiwa wananchi wa kaskazini sasa wanaishi katika Mikao yote ya Tanania, si jambo la maana wao wakahesabiwa kama ni wabaguzi kwa misingi ya asili au ujamaa.

"Tunachotaka kukisafanya baadhi ya wananchi wa Mikao ya Kaskazini ni kumuasi baba wa Taifa marehemu Mwalimu julius Nyerere, hakutuacha tukiwa tumegawanyika , tumeishi miaka yote hatukuongozwa kwa ukabila au udini, chadema acheni kwasabahu hilo ni balaa au janga katika jamii "alisema Raib.

Jumla ya wanachama wapya 103  walijiunga na chama cha mapinduzi pia shaka alipata nafasi ya kuangalia mechi ya soka kati ya timu za kata za makiidi na mahare wilaya ya Rombo.

Mfanyabiashara Auawa gesti Kwa Kuchomwa Kisu


Mfanyabiashara wa mazao, Eliusta Peter(40),   amefariki dunia baada ya kuchomwa na kitu chenye ncha kali shingoni akiwa katika  nyumba ya kulala wageni wilayani Kilombero.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei alisema tukio hilo lilitokea   Aprili 22  baada ya  wahudumu wa nyumba  ya wageni ya  Sayari kubaini   maiti katika chumba namba mbili.

Inadawa Aprili 20 mwanamke huyo  akiwa na kijana mmoja ambaye  jina lake limehifadhiwa kwa ajili ya uchunguzi, walifika kwenye nyumba hiyo na kuchukua chumba kimoja wakisema  wao ni wafanyabiashara wa mazao.
 
“Mwili wa marehemu uligundulika ukiwa kwenye nyumba ya kulala wageni iitwayo Sayari chumba namba mbili   saa 11 jioni na ulipochunguzwa ikagundulika kuwa kifo kilisababishwa maumivu ya jereha,”alisema Matei.

Mwanamke huyo  alikuwa na jeraha   kushoto mwa bega lake lililotokana na kuchomwa na kitu chenye ncha kali

Matei  alisema kwa taarifa walizozipata  bila shaka kijana aliyekuwa naye  anahusika na mauaji hayo.

Wakati huo huo, jeshi la polisi wilayani Kilosa limemkamata Rogasian Jeremia kwa tuhuma za kumshambulia mkewe,   Faustina Sizayi(25) kwa kumkatataka kwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake.

Mtuhumiwa alikamatwa akiwa anajihusisha na kazi ya ulinzi wa maduka baada ya polisi kumsaka kwa muda mrefu na ndipo Aprili  24  alikamatwa  baada ya polisi kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema.

Naibu Spika Achafua Hali ya Hewa Bungeni Baada ya Kumwita Mbunge wa Ukawa BWEGE

Naibu Spika Tulia Ackson, ambaye katika vikao vya Bunge anatakiwa kusimamia mijadala kwenye chombo hicho cha kutunga sheria, jana alizua kizaazaa baada ya kumuelezea mbunge wa Kilwa Kusini (CUF), Selemani Said Bungara kuwa ni bwege, akimtaka aache kuonyesha hali hiyo.

Kwa mujibu wa toleo la pili la Kamusi ya Kiswahili Sanifu (Oxford) la mwaka 2004, neno bwege linamaanisha “mtu mjinga, mpumbavu, bozi, fala gulagula”.

Kitendo cha kutumia neno bwege kumuelezea mbunge huyo kilisababisha wapinzani wacharuke, na kuibua bungeni kesi ya mtu aliyefunguliwa mashtaka mkoani Arusha kwa kosa la kumuelezea Rais John Magufuli kuwa ni bwege.

Bila ya kuruhusiwa, mmoja alifungua kipaza sauti na kusema: “Hatimaye msamiati wa bwege watua bungeni sasa kutumika rasmi. Futa lugha ya kuudhi; bwege bwege.”

Hata hivyo, wabunge hao wa upinzani hawakushinikiza Dk Tulia kufuta kauliz yake, lakini baadaye wakiwa nje ya ukumbi waliponda kitendo hicho cha kiongozi huyo wa Bunge ambaye aligombea uspika kwa tiketi ya CCM kabla ya kujitoa na muda mfupi baadaye kuteuliwa na Rais Magufuli kuwa mbunge na hivyo kupata sifa ya kugombea nafasi hiyo ya naibu spika.

Dk Ackson aliamsha tafrani hiyo saa 5:48 asubuhi baada ya Bungara, ambaye ni maarufu kwa jina la Bwege, kusimama bila kufuata kanuni za Bunge, kupinga maelezo ya Waziri wa Habari, Nape Nnauye juu ya uamuzi wa Serikali kusitisha shughuli za Bunge kurushwa moja kwa moja na vituo vya televisheni nchini.

“Na wewe Mheshimiwa Bwege, hebu kaa chini. Usionyeshe ubwege wako hapa,” alisema Dk Ackson kumzuia mbunge huyo asiendelee kuzungumza wakati mjadala ukianza kuwa mkali.

Mjadala huo uliendelea bila ya wapinzani kuhamaki, lakini baada ya Nape kutoa taarifa akieleza kuwa uamuzi wa kuanzisha studio za Bunge ulifanywa na Bunge la Kumi ambalo yeye hakuwamo, ndipo wapinzani walipokumbusha kauli hiyo ya naibu spika.

“Bunge linaonyeshwa asubuhi na kurudiwa kuonyeshwa usiku na kuna wanahabari hapa Dodoma wana kamera zao na wanaripoti bunge hili. Tusitumie bunge hili kupotosha,” alisema Nape kabla ya mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa kuingilia kati.

Msigwa: Hii ni taarifa au hotuba? 
Spika: Msigwa jifunze kusikiliza kwanza, unaipokea taarifa yake ama vipi?

Msigwa: Taarifa yake naikataa kwa sababu anasema uongo. Leo na wewe umemuita mtu bwege. Kuna mtu kule Arusha alimuita Rais Magufuli bwege na akapelekwa mahakamani. Na wewe tutakupeleka mahakamani.

Mkazi huyo wa Arusha, Isaack Habakuk Emily alipandishwa kizimbani takribani wiki mbili zilizopita akikabiliwa na shtaka la kumuita Rais kuwa ni bwege.

Msigwa alisema Bunge “nalo ni jipu” kwa kuwa haliwezi kuishauri Serikali kutokana na kufanya maamuzi bila ya kushirikisha makamishna wake, akitoa mfano wa chombo hicho kurejesha Sh6 bilioni serikalini ambazo zilibanwa kwenye matumizi yaliyoelezewa kuwa hayakuwa muhimu.

Baada ya Msigwa kumaliza kuchangia, alifuatia mbunge wa viti maalumu (Chadema), Tunza Malapo ambaye aliungana kauli na Msigwa na kumponda Nape na uamuzi wa Serikali.

Wakati Malapo akiendelea kuchangia, alisimama Khatibu kutoa taarifa.

“Kwa taarifa yako wewe Malapo aliyelishauri Bunge kutorushwa live ni Nape vuvuzela,” alisema.

“Kwani kuanzisha studio za Bunge maana yake ni Bunge kutorushwa moja kwa moja?”

Wakizungumzia tukio hilo la asubuhi, mbunge wa Kalenga (CCM), Godfrey Mgimwa alisema Dk Tulia alighafilika wakati akitoa kauli hiyo baada ya kurushiwa maneno mara kwa mara na wabunge wa upinzani, tena bila kufuata kanuni na taratibu za kibunge.

“Kwanza mtu mwenyewe (Bungara) huwa anapenda kuitwa bwege sasa kama ukiamua kumuita bwege utakuwa umekosea?” alihoji.

Alisema mara nyingi huibuka mvutano bungeni kwa sababu baadhi ya wabunge hawataki kuzingatia kanuni za chombo hicho cha kutun ga sheria.

Mbunge wa Moshi Vijijini (Chadema), Antony Komu alisema: “Kauli iliyotolewa na Naibu Spika inaonyesha wazi kuwa ni kiongozi anayekiuka misingi, taratibu na kanuni za Bunge. Tazama anatukana watu tu bila kujali jambo lolote, hii si sawa kabisa.”

Alisema Bunge linapaswa kuongozwa kwa haki na si kama ilivyo sasa ambayo inawafanya wabunge wa CCM waonekane kuwa na haki zaidi ya upinzani.

“Mfano (mbunge wa Tarime Vijijini-Chadema, John) Heche aliomba mwongozo akanyimwa ila Dk Kigwangalla akapewa,” alisema.

Kwa takribani wiki moja Bunge lilikuwa limepoa kutokana na wabunge wa vyama vya upinzani kususia kuchangia mjadala wa hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, lakini jana walishiriki kwenye mjadala wa wizara ya Ofisi ya Rais na kurejesha uhai kwenye chombo hicho.

Katika hoja zao jana, wabunge hao walijikita zaidi kuponda Serikali ya Awamu ya Tano kuwa inakiuka kanuni za utawala bora na kupinga uamuzi wake wa kusitisha matangazo ya Bunge, jambo lililomlazimu Nape kusimama mara kwa mara kutetea uamuzi wa Serikali, huku Dk Ackson akitoa ufafanuzi wa kanuni za Bunge.

Mara zote ambazo Nape na Dk Ackson walikuwa wakitoa ufafanuzi wao, walizomewa na wabunge hao wa upinzani huku mbunge wa Konde (CUF), Khatibu Said Haji akimfananisha Nape na “vuvuzela” kwa maelezo kuwa ndiye aliyeishauri Serikali kusitisha matangazo hayo. 

Akichangia mjadala huo, Mchungaji Msigwa alisema utawala bora na unaozingatia sheria hauanzi na bajeti, bali huanza na utawala bora.

“Tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, dhana nzima ya utawala bora haionekani. Utawala bora ni kuongoza nchi kwa ufanisi, tija na kwa uwazi, uadilifu, uwajibikaji na ushirikishwaji wa watu kwa kufuata utawala wa sheria,” alisema.

Alisema ni ajabu Ofisi ya Rais-Utawara Bora kuomba bajeti ya Sh800 bilioni wakati nchi haina utawala bora. Alirejea kauli ya kiongozi wa upinzani bungeni, Freeman Mbowe kuwa Serikali inaongozwa bila ya maamuzi yake kuwekwa kwenye Gazeti la Serikali.

“Walikuwa wanafanya kazi kama sisi tu mawaziri vivuli wa upinzani.Wanatoa maagizo wakati hawapo kisheria. Huu si utawala bora,” alisema Mchungaji Msigwa.

Alisema licha ya jambo hilo kubainika wazi Bunge lilikaa kimya huku akidai kuwa hata baadhi ya mawaziri walikuwa wanajua jambo hilo, na kwamba wanapokuwa nao katika mgahawa wa Bunge, wamekuwa wakiponda na kuukosoa utendaji kazi wa Serikali ya Rais Magufuli.

“Mawaziri mnakuwa kama vinyonga. Kwenye chai mnasema ukweli, mkija bungeni mnakaa kimya.Huwa tunawarekodi na mkibisha tutataja mmoja mmoja humu ndani,“ alisema Msigwa huku akimtaja Naibu Waziri wa Afya, Dk Hamisi Kigwangalla kuwa ni mmoja wa mawaziri hao baada ya waziri huyo kusimama kuomba mwongozo, kupinga kauli ya mbunge huyo.

Dk Kigwangalla alitumia kanuni 68 (7) na 63 (1) kuomba mwongozo, akimtaka Mchungaji Msigwa athibitishe kauli yake kwa kuwataja kwa majina mawaziri wanaopingana na uongozi wa Serikali.

Dk Ackson naye alitoa ufafanuzi akinukuu kifungu cha 63 (1) (2), kinachomtaka mbunge kuthibitisha jambo analolisema hapohapo ama apewe muda na kwamba atatoa maelezo ya kuwataka Dk Kigwangalla na Mchungaji Msigwa kuwasilisha ushahidi wao.

Msigwa: Mbona Kigwangalla unajihisi mwenye hatia? 
Dk Ackson: Msigwa unaongea na kiti usibishane na mbunge.

Msigwa: Mheshimiwa Spika wakati wa kuchangia tunakuwa na taarifa sio mwongozo ila nashangaa huyu (Dk Kigwangalla) kaomba mwongozo kapewa. Ila tunaendelea tu ila kiti bado kinayumba.

Dk Ackson: Mbunge anaweza kukosea na wengi tu hukosea. Ametaja kanuni zinazohusu utaratibu naomba tusiendelee kujibizana.

Akiendelea na mjadala huo Mchungaji Msigwa alisema Bunge la Tisa na la Kumi yaliendeshwa kwa uwazi mkubwa tofauti na Bunge la Kumi na Moja, kwamba hata utawala wa Serikali ya Awamu ya Nne ulikuwa haubani demokrasia na kuzuia matangazo ya Bunge kurushwa moja kwa moja.

“Bunge ni mkutano wa wazi wa wananchi wote, lakini Serikali hii inaanza kuminya na kuweka siri. Huu si mkutano wa unyago, tunaongelea matumizi ya fedha za Watanzania,” alisema.

“Serikali inayokandamiza uwazi ni Serikali iliyojaa uoga na inayoficha madudu. Mnasimama na kusema mnakusanya fedha za kuvunja rekodi sasa mnaficha nini kuwaonyesha Watanzania hiki mnachokifanya?”

Huku akiipongeza Serikali iliyokuwa ikiongozwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete, Mchungaji Msigwa alisema pamoja na udhaifu wake, ilikuwa haizuii watu kuzungumza na kusema ukweli.

“Nyinyi mmekuja na ‘hapa kazi tu’, lakini hamtaki kukosolewa. Wakati tunamkosoa Kikwete wabunge wa CCM mlikaa kimya na kutuzomea, leo mnaufyata na inaonekana hata Dk Magufuli akidondosha kijiko, mtasimama na kupiga makofi kwa sababu ya uoga wenu,” alisema Mchungaji Msigwa na kuwataka wabunge kuhoji mambo kwa maslahi ya wananchi. 

Rufaa Kupinga Kuachiwa Huru Abdallah Zombe na Wenzake kusikilizwa Leo

Abdallah Zombe (kushoto) akiwa na wakili wake, Richard Rweyongeza katika Mahakama ya Rufaa, Dar es Salaam
****
Mahakama ya Rufaa leo inatarajiwa kusikiliza rufaa ya kupinga kuachiwa huru kwa aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam (RCO) Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Abdallah Zombe na askari wenzake wanane waliokuwa wanakabiliwa na mashitaka ya mauaji.

Rufaa hiyo inatarajiwa kusikilizwa mbele ya jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Bernard Luanda, wengine ni Jaji Sauda Mjasiri na Jaji Semistocles Kaijage. 

Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), alikata rufaa mwaka 2013, akipinga hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam iliyowaachia huru Zombe na wenzake, baada ya kuwaona hawana hatia katika kesi ya mauaji ya watu wanne iliyokuwa inawakabili.

Katika rufaa hiyo, DPP anadai kuwa Jaji Salum Massati alikosea kuwaachia huru washitakiwa hao kwa sababu kulikuwa na ushahidi wa kutosha kuwatia hatiani wote. 

Mbali na Zombe, wajibu rufaa wengine ni ASP Christopher Bageni, ASP Ahmed Makelle, Konstebo Jane Andrew, Konstebo Emanuel Mabula, Konstebo Michael Shonza, Koplo Abeneth Salo, Koplo Rajabu Bakari na Koplo Festus Gwabisabi.

Katika kesi ya msingi inadaiwa Januari 14, 2006, katika msitu wa Pande uliopo Mbezi Luis, Dar es Salaam Zombe na wenzake waliwaua kwa makusudi wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Morogoro, Mathias Lunkombe, Sabinus Chigumbi na ndugu yake Ephrahim Chigumbi, pamoja na dereva teksi Juma Ndugu.

Baada ya kusikiliza kesi hiyo, Agosti 17, 2009, Jaji Massati aliwaachia huru washitakiwa kwa kuwa upande wa Jamhuri ulishindwa kuthibitisha mashitaka dhidi yao bila kuacha shaka na Mahakama ikiwaona hawana hatia kwa makosa yaliyokuwa yanawakabili.

Oktoba 6, 2009, DPP alikata rufaa Mahakama ya Rufani, akipinga hukumu hiyo kwa madai kuwa Jaji Massati alikosea kuwaachia huru washtakiwa hao, pia kulikuwa na ushahidi wa dhahiri na wa kimazingira unaotosha kuwatia hatiani washtakiwa wote.

Hata hivyo Mei 8, 2013 Mahakama ya Rufaa ilitupilia mbali rufaa hiyo kutokana na dosari za kisheria zilizobainika kwenye rufaa, lakini DPP alipeleka maombi Mahakama Kuu ili aruhusiwe kukata tena rufaa nje ya muda. 

Mahamaka Kuu ilikubali maombi yake, akakata tena rufaa inayotarajiwa kusikilizwa leo.

Trump Achekwa Baada Ya Kushindwa Kulitamka Jina la Nchi yetu Tanzania

Mgombea wa urais kupitia chama cha Republican nchini Marekani ambaye amekuwa akiongoza kwenye kinyang’anyiro hicho, Donald Trump amejikuta akikosolewa vikali kuhusu upeo wake juu ya sera za nje pale aliposhindwa kulitamka bayana jina la Tanzania.

Drump ambaye Jumanne aliyopita alivuna ushindi wa kishindo kwenye majimbo yote manne yaliyopiga kura za mchujo alijikuta akitumbukia kwenye kadhia hiyo wakati akielezea vipaumbele vya Marekani kuelekea mataifa ya kigeni.

Alikuwa akigusia juu ya mashambulizi ya mabomu yaliyotokea katika ubalozi wa Marekani nchini Tanzania na Kenya na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali huku watu kadhaa wakipoteza maisha.

Akiwa katika hali ya kujiamini, Trump alisema kuwa iwapo ataingia madarakani moja ya vipaumbele vyake ni kuendelea kutetea masilahi ya Marekani na kudhihirisha hilo aliamua kutolea mfano mashambulizi hayo ya kigaidi.

Lakini wakati akilitaja jina la Tanzania, mfanyabiashara huyo alijikuta akigusa hisia za wengi pale alipolitaja jina hilo kinyume na inavyotamkwa. “ Ona mashambulizi yaliyotokea katika miaka ya 1990 katika ubalozi wetu nchini Tan-ZAY-nee-uh”.

Matamshi hayo yalizusha mjadala mkubwa huku baadhi ya wakosoaji wake wakiingia kwenye mitandao ya kijamii na kuanza kumuelezea kama ni mtu asiyekuwa na upeo mkubwa kuhusu siasa za kimataifa.

Baadae kambi ya kampeni ya Trump ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari ikisema kuwa kuteleza kwa mgombea wao katika matamshi ya jina halisi la Tanzania hakumaanishi kuwa uwezo wake kuhusu masuala ya usalama,diplomasia ya kimataifa na biashara ya kimataifa ni wa kutiliwa mashaka.

CHADEMA Yatangaza Kutoshiriki Kura ya Maoni ya Katiba Mpya

DK. Vincent Mashinji Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (chadema), amesema kuwa Katiba Mpya inayotokana na maoni ya wananchi ndiyo msingi imara pekee unaoweza kuweka mifumo na taasisi kwa ajili ya maendeleo ya kweli yatakayogusa maslahi ya Watanzania wote badala ya nchi kuongozwa na kauli za viongozi.

Kutokana na umuhimu huo wa kuzingatia maoni ya wananchi yanayobeba matakwa yao katika mchakato wa Katiba Mpya, amesema kuwa Chadema hakitashiriki kura ya maoni ya Katiba Mpya Inayopendekezwa ambayo ilipitishwa na Bunge Maalum la Katiba baada ya kubadili na kuondoa mapendekezo yaliyotolewa na wananchi kwenye Rasimu ya Pili ya Katiba Mpya.

Badala yake, Chadema kitaendelea kuweka agenda ya kupigania Katiba Mpya na bora katika vipaumbele vyake, kwa sababu itatibu vidonda na kumaliza makovu yaliyoko katika jamii kutokana na matatizo mbalimbali kama vile ukosefu wa haki, migogoro ya ardhi, wananchi kukosa huduma za msingi za kijamii zikiwemo elimu, maji na afya.

Dkt. Mashinji aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam alipoukaribisha ujumbe wa Chama cha Centre Party cha Norway uliofika ofisini kwake jijini Dar es Salaam kutia saini makubaliano ya ushirikiano kati ya vyama hivyo kwenye Mradi wa Elimu ya Demokrasia awamu ya pili unaofanyika Wilaya ya Mtwara Vijijini.

Dkt. Mashinji pia amekishukuru chama hicho kwa kusaidia kutoa elimu ya uraia kwa Watanzania hususani maeneo ya vijijini katika mradi ambao unahusisha vyama vyote vya siasa vyenye uwakilishi ndani ya Bunge, huku akisisitiza kuwa Chadema kiko tayari kwa ushirikiano unaozingatia maslahi na matakwa ya wananchi hasa katika kukuza uelewa wa kudai haki, demokrasia na uongozi bora ndani ya nchi.

“Suala la Katiba Mpya inayotokana na maoni ya wananchi kama ilivyowasilishwa kwenye rasimu ya pili na Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya ni agenda muhimu kwa Watanzania wapenda nchi yao na sisi ni kipaumbele kwa mwaka huu na kuendelea hadi hapo nchi yetu itakapopata Katiba Mpya ya Wananchi.

“Jana na leo tumewasikia baadhi ya viongozi wa serikali wakisema kuwa wanajiandaa kuitisha kura ya maoni…hatutashiriki kura ya maoni ya Katiba Mpya Inayopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba. Tunajua Watanzania wengi wanataka Katiba Mpya iliyotokana na maoni yao, si ile iliyochakachuliwa bungeni.

“Katiba Mpya iliweka masuala kuhusu haki za wananchi, kuimarisha misingi na kuweka mifumo ya demokrasia na uongozi bora, walau kwa kuanzia. Hatuwezi kusema sasa tutatumia mikakati gani kuwahamasisha Watanzania kuidai Katiba Mpya…tutajua namna ya kuvuka tukishafika mtoni,” Alisema

Aidha, Katibu Mkuu Dkt. Mashinji alisisitiza kuwa suala la nchi kuwa na misingi na mifumo imara ya demokrasia na uongozi bora ni muhimu kwa Tanzania, katika wakati ambapo nchi inaelekea kwenye uchumi mkubwa wa nishati ya gesi na mafuta, akisema vinginevyo ni hatari iwapo taifa lenye utajiri mkubwa wa rasilimali, litaendelea kuwa na wananchi waliokata tamaa kutokana na mfumo mbovu uliopo.

Kwa upande wake ujumbe huo uliokuwa ukiongozwa na Katibu Mkuu wa Centre Party, Knut Olsen, ulisema kuwa chama hicho kinashukuru kwa mradi huo kuingia katika hatua ya pili kuanzia mwaka 2016-2019 huku hatua ya kwanza ikiwa na mafanikio makubwa katika jamii ya wananchi wa maeneo ya pembezoni.

“Kama unavyojua, mradi huu kupitia TCD unahusisha vyama vyote vyenye uwakilishi ndani ya bunge, na lengo letu ni kuwajengea uwezo viongozi wa vyama hasa wanawake na vijana katika ngazi ya jamii kwenye vitongoji, vijiji, kata na bunge ili waweze kushiriki mchakato wa maamuzi. Tunatarajia kuendelea kupata ushirikiano katika hatua ya pili,”alisema Inger Bigum, ambaye ni Meneja wa Mradi hapa nchini.

Wengine waliokuwa katika ujumbe huo wa Centre Party ni pamoja na Vijana Sara Hamre Katibu Mkuu wa, Katibu Mkuu wa Wanawake, Eline Stokstad-Oslan na Kristin Madsen Katibu Mkuu wa Wazee.

Mradi huo wa Elimu ya Demokrasia katika Wilaya ya Mtwara Vijijini unaohusisha vyama vyenye uwakilishi bungeni kupitia Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) chini ya ufadhili wa chama hicho, katika awamu ya kwanza ulihusisha kata za Msangamkuu, Nanyamba, Ziwani na Mbembaleo na katika sasa awamu ya pili utakuwa katika kata za Mkunwa, Tangazo, Mayanga na Madimbwa.